Mpango Mkakati wa TAG Miaka 10 ya Mavuno - Tanzania kwa Yesu



TANZANIA ASSEMBLIES OF GOD

TAMKO LA KUJIWEKA WAKFU KWA AJILI YA MIAKA 10 YA MAVUNO – TANZANIA

(DECADE OF HARVEST TANZANIA 2009 – 2018)

Kwa kuwa TUNAAMNI katika Agizo Kuu ambalo linatutuma kuhubiri habari njema ulimwenguni kote na kwa kila kiumbe (Mathayo 28:19); Kwa kuwa TUNAAMINI kuwa sasa ni wakati wa mavuno kwa taifa la Tanzania; Kwa kuwa TUNAAMINI kuwa tamko la Halmashauri Kuu lilipitishwa na Baraza la Waangalizi na kisha kuthibitishwa na Baraza Kuu (Kupitia Conference za Majimbo yote kumi). Kwamba miaka hii kumi ya 2009-2018, kuwa ni miaka kumi ya mavuno. Tukiwa tumeisikia vema sauti ya Roho Mtakatifu akiongea na mioyo yetu kama watumishi viongozi tuliojitoa kikamilifu na wenye maono makubwa. Sisi Kanisa la Tanzania Assemblies of God, tunatamka tamko la kujiweka WAKFU kwa Bwana na UWEZA wa NGUVU ZAKE kama ifuatavyo:-

TUNAJIWEKA WAKFU kufunga na kuomba na kuendelea, na kuhubiri mahubiri ya Kipentekoste tukitazamia umwagiko wa Roho Mtakatifu katika nchi yote ya Tanzania. Tukiomba sawasawa na 2Nyakati 7:14; kwa ajiil ya uamsho mkuu Tanzania unaoambatana na nguvu za Kipentekoste, mahubiri yenye nguvu na udhihirisho na utendaji kazi wa Roho Mtakatifu kwa kiwango kamili katika kanisa lake (Mdo. 1:8).

TUNAJIWEKA WAKFU SISI WENYEWE kwa makusudi kabisa kumfikia kila mtu katika Tanzania kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Miji yote kwa ushuhuda wa Injili kamili (Yesu anaokoa, Yesu anaponya, Yesu anajaza Roho Mtakatifu na Yesu anarudi tena). Ili lengo hili lifanikiwe, tutatumia kila mbinu ya kuhubiri; Radio, Televisheni, Maandiko, Tovuti, Mtu kwa Mtu, Michezo, Mikutano, huduma maalumu na vyanzo vingine halali. Tunaunganisha nguvu zetu katika taifa zima kama kanisa, pamoja na washirika wenza ndani na nje ya nchi, watakaosimama nasi katika kuvuna mavuno haya na kuyaleta ghalani.

TUNATHIBITISHA KUJIWEKA KWETU WAKFU kwa kuanzisha makanisa imara, kuwafunza na kuwawezesha wote ambao Bwana anawaita katika mavuno haya. Kwa hiyo tumeazimia kuimarisha huduma ya kanisa inayoweza kufanya umisheni katika maeneo yasiyofikiwa ndani na nje ya mipaka ya nchi.

TUNAWAITA WATUMISHI WOTE wa TAG waanzishe maombi na maombezi ya kipekee kwa ajili ya miaka 10 ya mavuno.

TUNAWAITA watumishi wote wa TAG waonyeshe uhai mpya na maono mapana ya kimisheni ikiambatana na kupeleka watumishi maeneo yasiyofikiwa ili Yesu Kristo ahubiriwe kwa kila mtu. TUNATANGAZA vita vya kiroho katika nchi nzima, tukishambulia wakuu na nguvu za giza katika ulimwengu wa Roho kama itamkwavyo katika Waefeso 6:12; tukijua ya kwamba sisi ni WASHINDI NA ZAIDI YA KUSHINDA kwa Yeye aliyetupenda (Rum 8:12).

TUNAAMINI kwa uweza wa Mungu tutatenda MAKUU hadi kufikia malengo yafuatayo: -

Ø  TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA UAMSHO utakaomwagika nchi nzima na kusababisha mafuriko makubwa ya utendaji wa Roho Mtakatifu kwa kanisa kama matokeo ya kujiweka wakfu na kuomba kusikokoma kwa washirika wote.
Ø  TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA WASHIRIKA 2,000,000 ifikapo mwaka 2018. Hii ina maana kila mshirika ni mtenda kazi kwa hiyo amlete mwongofu mpya mmoja au zaidi kila mwaka.
Ø  TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA MAKANISA 10,000 ifikapo mwaka 2018. Kila kanisa lizae kanisa moja au zaidi kila miaka mitatu.
Ø  TUNAMWAMINI MUNGU KUWA NA WACHUNGAJI 10,000 ifikapo 2018. Kila Mchungaji aliyepo azae mchungaji mmoja au zaidi na kuwawezesha kusoma chuo cha utumishi.
Ø  TUNAMWAMINI MUNGU KWAMBA KILA JIMBO LITAKUWA NA CHUO CHA KUPANDA MAKANISA, pia kuviongeza, kuvipanua na kuviboresha vyuo vyote vilivyopo kwa lengo la kuharakisha kasi ya kuvuna na kutunza mavuno.
Ø  TUNAMWAMINI MUNGU KUWA, katika kanisa kuwajibika kwa jamii kila Jimbo na Idara itaanzisha au shule ya chekechea ama msingi au sekondari ama vyote kwa pamoja.
Ø  TUNAMWAMINI MUNGU kufanya zaidi ya yale tunayoweza kufikiri na kuwaza huku tukiendelea kukusanya mavuno kwa uaminifu.

KWA KUTEKELEZA HAYO:
·         Neno la Mungu litakuwa mwongozo wetu na mpango wetu wa kazi
·         Kweli za Kibiblia zisizoyumbishwa, zisizopunguzwa zitakuwa jumbe zetu za Injili
·         Roho wa Mungu atakuwa mwezeshaji na nguvu Yetu ya huduma
·         Damu ya Bwana Yesu Kristo inatuhakikisha ushindi.
·         Kanisa litakuwa kiroho, kiidadi, kijiografia, kiufanisi, na kwa wana wapotevu kurudi kwa Bwana Yesu.

KAULI MBIU YETU: MIAKA KUMI YA MAVUNOOO!!! TANZANIA KWA YESU.
TANZANIA KWA YESUUU!!! MIAKA KUMI YA MAVUNO.

Mpango Mkakati wa TAG Miaka 10 ya Mavuno - Tanzania kwa Yesu Mpango Mkakati wa TAG Miaka 10 ya Mavuno - Tanzania kwa Yesu Reviewed by Unknown on 3:20 PM Rating: 5

1 comment:

ads
Powered by Blogger.